Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya yashambuliwa, 13 wauawa na kujeruhiwa
(last modified Tue, 25 Dec 2018 14:49:32 GMT )
Dec 25, 2018 14:49 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya yashambuliwa, 13 wauawa na kujeruhiwa

Kwa akali watu watatu wameuawa akiwemo mtumishi wa umma wa ngazi za juu, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia jengo lenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya katika mji mkuu Tripoli.

Duru za kiusalama zimedokeza kuwa, huenda waliotekeleza hujuma hiyo ya leo Jumanne ni wanachama wa kundi lenye mfungamano na genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).

Habari zinasema kuwa, magaidi hao waliingia katika jengo la wizara na kisha kuanza kufyatua risasi ovyo, kabla ya wawili miongoni mwao kujiripua na kuaga dunia papo hapo, huku wa tatu akiuawa na walinzi wa jengo hilo.

Wizara ya Afya ya Libya imesema watu kumi wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo kufuatia mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini na magaidi hao.

Magenge ya wabeba silaha Libya

Inaarifiwa kuwa, msemaji wa genge hilo la kigaidi kwa jina Abdulrahman Mazoughi ni miongoni mwa watu waliouawa katika hujuma hiyo dhidi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya.

Libya hivi sasa imegawanyika na kuwa na serikali mbili tofauti, mbali na kukosa utulivu katika kipindi cha miaka saba sasa tangu alipopinduliwa na kuuawa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.