Mo Ibrahim: ICC imfutie mashitaka Rais wa Sudan iwapo ataachia ngazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50763-mo_ibrahim_icc_imfutie_mashitaka_rais_wa_sudan_iwapo_ataachia_ngazi
Bilionea mashuhuri mzawa wa Sudan, Mohammed Ibrahim amesema Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inapaswa kumuondolea mashitaka Rais Omar al-Bashir wa Sudan iwapo atakubali kujiuzulu, kama anavyoshinikizwa na wananchi wanaofanya maandamano dhidi yake tangu mwezi uliopita.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 09, 2019 23:20 UTC
  • Mo Ibrahim: ICC imfutie mashitaka Rais wa Sudan iwapo ataachia ngazi

Bilionea mashuhuri mzawa wa Sudan, Mohammed Ibrahim amesema Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inapaswa kumuondolea mashitaka Rais Omar al-Bashir wa Sudan iwapo atakubali kujiuzulu, kama anavyoshinikizwa na wananchi wanaofanya maandamano dhidi yake tangu mwezi uliopita.

Mjasiriamali huyo ambaye ni mlezi wa Tuzo ya Kifahari ya Mo Ibrahim ambayo hutunukiwa viongozi wa Afrika walioonesha ukomavu wa kidemokrasia katika utawala wao amesema, "Binafsi napenda kuona watu wakiadhibiwa kutokana na madhambi waliyoyafanya. Lakini iwapo gharama ya kukubali kujiuzulu Rais wa Sudan ili kukomesha umwagikaji wa damu katika nchi hiyo ya Kiafrika ni kufutiwa mashitaka na ICC, nafadhilisha jambo hilo lifanyike."

Makumi ya waandamanaji wameuawa na mamia ya wengine kutiwa nguvuni tangu wananchi wa maeneo mbalimbali ya Sudan walipoanza maandamano ya kupinga sera za kiuchumi za serikali ya nchi hiyo tarehe 19 mwezi uliopita wa Disemba. 

Hivi sasa waandamanaji hao wanamtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1993 ajiuzulu.

Rais Bashir wa Sudan

Rais wa Sudan anatuhumiwa na ICC kuwa alihusika na jinai na mauaji ya kimbari huko Darfur magharibi mwa nchi hiyo mwaka 2003.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi imetoa waranti wa kukamatwa al-Bashir mara mbili, mwaka 2009 na 2010. Hata hivyo nchi nyingi hususan za Afrika zimekataa kumkamata na kumkabidhi kwa ICC rais huyo wa Sudan, alipozitembelea nchi hizo.