Jan 15, 2019 14:40 UTC
  • Watu 12 wauawa katika hujuma ya kigaidi nchini Msumbiji

Kwa akali watu 12 wameuawa katika shambulizi la kigaidi kaskazini mwa Msumbiji.

Duru za kiusalama zimeripoti kwamba, akthari wa wahanga wa shambulizi hilo lililotokea katika eneo la Cabo Delgado ni abiria waliokuwa katika usafiri binafsi na mabasi ya umma.

Kadhalika watu kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la kigaidi. Haya yanajiri siku chache baada ya watu wengine kadhaa kuuawa katika shambulizi la kigaidi.

Jumamosi iliyopita, watu wanne waliuawa baada ya kuviziwa na genge la kitakfiri katika mji wa Manilha mkoani Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji.

Maafisa usalama mkoani Cab Delgado

Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Baada ya kushadidi hujuma hizo, serikali ya Msumbiji ilituma wanajeshi na polisi katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Tanzania na tayari imewakamata mamia ya washukiwa.

Tags