Tanzania kuchunguza uchinjaji wa watoto 10 Njombe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51197-tanzania_kuchunguza_uchinjaji_wa_watoto_10_njombe
Serikali ya Tanzania imesema itachunguza tukio la kusikitisha la watoto 10 kupoteza maisha baada ya kuchinjwa katika eneo la Njombe.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jan 29, 2019 10:25 UTC
  • Tanzania kuchunguza uchinjaji wa watoto 10 Njombe

Serikali ya Tanzania imesema itachunguza tukio la kusikitisha la watoto 10 kupoteza maisha baada ya kuchinjwa katika eneo la Njombe.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Serikali inalaani mauaji hayo na imejipanga kuhakikisha inadhibiti na kutokomeza mtandao huo unaojihusisha na mauaji hayo ya kikatili ya watoto.

Amesema tukio hilo halitopita hivi hivi na kwamba serikali tayari imeshawakamata baadhi ya watuhumiwa wa mauaji hayo kupitia vyombo vya ulinzi na usalama likwemo jeshi la polisi.

Akizungumza katika mazishi ya watoto watatu kati ya 10 waliouawa, ambao walikuwa kutoka familia moja, Masauni amesema mtu yoyote ambaye anajishughulisha na mauaji dhidi ya binadamu wakiwemo watoto wadogo atakamatwa. Akizungumza juu ya mauaji hayo Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kibena huko Njombe Barnabas Baraka amesema vifo vya watoto hao vimetokana na kushambuliwa na vitu vizito na vyenye makali maeneo ya kichwani huku mmoja akiwa amekatwa sikio la kulia.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiwa katika mazishi ya watoto waliochinjwa Njombe

Watoto hao wameuawa katika mazingira ya kutatanisha baada ya kutekwa nyara na inaaminika kuwa chanzo ni itikadi za kishirikina. 

Mauaji yanayotokana na itikadi za kishirikina nchini Tanzania ni kitu cha kawaida ambapo katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, albino, na vipara.