Mkutano wa wakuu wa EAC hatimaye wafanyika Arusha, Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51264-mkutano_wa_wakuu_wa_eac_hatimaye_wafanyika_arusha_tanzania
Marais wanne kati ya sita wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, wamewasili Arusha Tanzania, kushiriki mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo ya kikanda ambao mwaka jana ulifutwa mara mbili ndani ya muda wa wiki tatu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2019 10:24 UTC
  • Mkutano wa wakuu wa EAC hatimaye wafanyika Arusha, Tanzania

Marais wanne kati ya sita wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, wamewasili Arusha Tanzania, kushiriki mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo ya kikanda ambao mwaka jana ulifutwa mara mbili ndani ya muda wa wiki tatu.

Mwenyeji Rais John Magufuli amewapokea marais wenzake Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda. Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi atawakilishwa na makamu wake wa kwanza, Gaston Sindimwo, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini, Nhial Deng Nhial akimuwakilisha Rais Salva Kiir.

Mbali na masuala ya utangamano, mkutano huo unatazamiwa kujadili uhasama kati ya Rwanda na Uganda, vita vya kibiashara miongoni mwa nchi wanachama, na pia mpango wa kuijumuisha Somalia katika jumuiya hiyo.

Mkutano huo wa marais wa nchi wanachama wa EAC ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini ulitazamiwa kufanyika Disemba 27 lakini ukaakhirishwa, wiki tatu baada ya ule wa kwanza uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 30 kufutwa baada ya Burundi kusema kuwa haitashiriki, kutokana na uhasama wa nchi hiyo na jirani yake Rwanda.

Wakuu wa EAc katika mkutano wa mwaka 2016

Burundi na Rwanda zimekuwa katika mzozo tangu kulipojiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Nkurunziza hapo tarehe 13 Mei 2015.

Wadadisi wa mambo wanasema kuakhirishwa mkutano huu muhimu wa marais wa EAC ni ishara ya kuendelea kuwepo migogoro na mpasuko mkubwa miongoni mwa nchi wanachama.