Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania azindua mahakama inayotembea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51369-rais_john_pombe_magufuli_wa_tanzania_azindua_mahakama_inayotembea
Rais John Magufuli wa Tanzania amezindua gari maalumu la mahakama inayotembea litakalosaidia kusikiliza kesi katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2019 09:12 UTC
  • Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania azindua mahakama inayotembea

Rais John Magufuli wa Tanzania amezindua gari maalumu la mahakama inayotembea litakalosaidia kusikiliza kesi katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam.

Uzinduzi wa gari hilo lenye teknolojia ya kisasa ndani yake na linalotumia umeme wa jua katika uendeshaji vifaa hivyo umefanyika leo katika maadhimisho ya Siku ya Sheria. Gari hilo limegharimu kiasi cha Shilingi milioni 470.82.

Gari hilo lenye television, kamera zenye uwezo wa kurekodi ushahidi wote kwa picha na sauti, kutoa msaada wa kuwabeba watu wenye ulemavu (lifti) na kipaza sauti kwa ajili ya kutangaza ratiba ya mahakama hiyo, linatazamiwa kusaidia uharakishaji wa kesi ambazo aghlabu zimekuwa zikirundikana katika mahakama za nchi hiyo.

Moja ya mahakama za jijini Dar es Salaam Tanzania

Kwa kuanzia gari hilo limetakiwa kutoa huduma katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mwanza kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya watu wanaoishi miji hiyo. Wakati huo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema kwamba, mahakama za nchi hiyo zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi 18,556 ili ziweze kuboresha utendajikazi wake kwa ufanisi. Amesema kuwa, licha ya upungufu huo idadi ya watumishi imeendelea kupungua siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali hivyo kuendelea kuongeza changamoto hiyo katika sekta hiyo. Akizungumzia suala la usikilizaji wa kesi kwa njia ya video, Profesa Juma amesema kuwa suala hilo linaweza kupunguza gharama za kumleta shahidi mahakamani na badala yake akaweza kusikilizwa akiwa mahabusu au gerezani. Ametolea mfano kuwa, Disemba pili mwaka jana Mahakama Kuu ya Biashara ilimsikiliza shahidi akiwa nchini Ufaransa kupitia njia ya video na hivyo ikawa imeokoa gharama za kumleta shahidi huyo Tanzania.