Feb 17, 2019 08:09 UTC
  • Askari 7 wa Niger wauawa katika mapigano na Boko Haram

Wanajeshi saba wa Niger wameuawa baada ya kambi yao kushambuliwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kusini mashariki mwa nchi karibu na mpaka wa Nigeria.

Taarifa ya jana Jumamosi ya Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo imesema wanajeshi saba waliuawa huku wengine sita wakijeruhiwa katika makabiliano hayo, yaliyotokea katika eneo la Chetima Wanou.

Bila kutaja idadi kamili, taarifa hiyo imesema wanamgambo kadhaa wa kigaidi waliuawa katika uvamizi huo, dhidi ya kambi ya jeshi kusini mashariki mwa nchi.

Mwezi uliopita, askari kumi wa Nigeria na Niger waliokuwa katika operesheni ya pamoja waliuawa na wanamgambo hao katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Wanajeshi wa Niger wakiwasaka wananchama wa Boko Haram

Hata hivyo siku mbili baadaye, leshi la Niger liliwaua zaidi ya wanachama 280 wa kundi hilo la kigaidi karibu na mpaka wa kusini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia operesheni ya ulipizaji kisasi ya siku kadhaa ya wanajeshi wa serikali dhidi ya magaidi hao.

Kundi hilo la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi katika nchi nne zinazopakana na Ziwa Chad za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon kwa muda mrefu sasa.

Nchi hizo nne zimeunda kikosi cha pamoja cha kupambana na magaidi hao, lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kuliangamiza genge hilo la wakufurishaji.

Tags