Waalgeria waandamana hadi hospitali alikolazwa Bouteflika nchini Uswisi
(last modified Sat, 09 Mar 2019 04:22:36 GMT )
Mar 09, 2019 04:22 UTC
  • Waalgeria waandamana hadi hospitali alikolazwa Bouteflika nchini Uswisi

Waalgeria wanaoishi nchini Uswisi wamefanya maandamano ya kupinga msimamo wa Rais Abdelaziz Bouteflika wa kugombea tena urais kwa muhula wa tano.

Kanali ya televisheni ya Al Hadath imeripoti kuwa Waalgeria walioko nchini Uswisi wameandamana hadi mbele ya jengo la hospitali moja ya mjini Geneva, mahali alikolazwa rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika akiwa anapatiwa matibabu.

Rashid Nikaz, mmoja wa wagombea urais wa Algeria, ambaye jina lake halikupitishwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo, naye pia ameshiriki katika maandamano hayo ya Geneva.

Kwa siku kadhaa sasa, wananchi wa Algeria wanaandamana katika miji mbali mbali ya nchi hiyo kupinga uamuzi wa Bouteflika wa kugombea tena urais ili kuweza kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa tano mfululizo.

Maandamano ya upinzani nchini Algeria

Hivi karibuni, kundi moja la viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kisiasa walitoa mwito wa kuakhirishwa uchaguzi huo wa rais ambao umepangwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi ujao wa Aprili.

Wapinzani wa kiongozi huyo wanasema, Bouteflika hana uwezo tena wa kuendelea kuongoza nchi kutokana na afya yake kudhoofika na kwa sababu ya kile wanachokiita ufisadi sugu na kukosekana mageuzi ya kiuchumi ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kinachopindukia asilimia 25 kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30 nchini Algeria.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82, anayetembea kwa kutumia kiti cha magurudumu amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.../