Chama tawala nchini Tanzania: Wanachama wa CCM waheshimuni wapinzani
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nchini Tanzania Dk Bashiru Ally amewataka wanachama wa chama hicho tawala nchini humo, kutowabeza wapinzani na badala yake kuheshimu alama za vyama vyote vya siasa kwa sababu vimesajiliwa kisheria.
Dk Bashiru ameyasema hayo leo wakati akizindua mkakati wa kukomaza na kuimarisha demokrasia kwenye mashina ulioandaliwa na chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Dodoma. Kadhalika amewataka wanachama wa chama hicho kutochoma wala kubeza alama za vyama hivyo na kwamba hivi karibuni kuna wafuasi wamechoma bendera na kupaka rangi ya chama chao ofisi za chama kingine. "Ni kosa kuparamia na kupaka rangi ofisi za vyama hivyo. CCM tusifanye hivyo ni kosa kisheria. Aidha ametaka wanachama wa CCM kuwa mfano bora na kwamba serikali ina wajibu wa kulinda vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria nchini humo.
Indhari ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi imekuja ikiwa ni siku chache tangu msaliji wa vyama vya siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi kuwatuhumu wafuasi wa chama cha ACT-Wazalendo kwa kuchoma moto bendera za chama cha Wananchi CUF visiwani Zanzibar na kudai kuwa anafuatilia suala hilo. Akijibu tuhuma hizo, Zitto Zuber Kabwe, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo kupitia mahojiano na mwandishi wa habari Maria Sarungi, alizitaja tuhuma za msajili wa vyama vya siasa kuwa za upendeleo na zisizozingatia usawa.
Alienda mbali zaidi na kusema: “Ni hivi karibuni tulishuhudia wafuasi wa CCM wakichoma kadi za chama cha ACT-Wazalendo, lakini hatukuona Bwana Mutungi akichukua hatua yoyote.” Alisema Zitto. Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa chama cha ACT-Wazalendo, amesema kuwa, wakati umefika kwa wananchi wa Pemba kuongeza nguvu ya kudai mabadiliko ili kujikwamua kiuchumi. Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini (magharibi mwa Tanzania) ametoa kauli hiyo leo Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba wakati akizungumza na waliokuwa wanachama wa CUF, ambao sasa wamejiunga na chama chake. Aidha amesema hali ya maisha ya wananchi wa Pemba ni duni jambo ambalo linapaswa kutazamwa kwa macho mawili na umakini.