Mar 24, 2019 03:12 UTC
  • Waziri ni miongoni mwa watu 15 waliouawa katika shambulizi la kigaidi Somalia

Kwa akali watu 15 wameuawa katika shambulizi la kigaidi la jana Jumamosi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Saqar Ibrahim Abdallah, Naibu Waziri wa Leba na Masuala ya Jamii wa Somalia ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo. Kapteni Osman Muhammed, afisa wa polisi mjini Mogadishu amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa maafisa usalama wametamatisha operesheni ya kulidhibiti jengo ambalo lilikuwa limeshambuliwa. 

Muhammad Hussein, mmoja wa makanda wa polisi nchini Somalia hapo jana alisema kuwa mripuko wa kwanza wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari ulijiri karibu na Wizara ya Kazi, ambapo majengo ya wizara nyingine pia yaliathirika.

Mripuko mwingine wa bomu ulitokea muda mfupi baada ya ule wa kwanza na ulifuatiwa na ufyatuaji risasi uliofanywa na washambuliaji.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kupitia msemaji wake wa operesheni za kijeshi, Abdiasis Abu Musab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya jana.

Wananchi wa Somalia wakikimbilia usalama wao baada ya kujiri mripuko wa bomu

Rais wa Somalia, Mohammed Abdullahi Farmajo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hassan Ali Khaire wametoa mkono wa pole kwa familia za waathiriwa wa shambulizi hilo la jana.

Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limekuwa likifanya juhudi zenye lengo la kuipindua serikali kuu ya nchi hiyo ambayo inapata himaya kutoka kwa askari wa Umoja wa Afrika AMISOM.

Tags