Misaada ya UNCHR yaanza kuwasili Msumbiji baada ya mafuriko
(last modified Thu, 28 Mar 2019 07:57:44 GMT )
Mar 28, 2019 07:57 UTC
  • Misaada ya UNCHR yaanza kuwasili Msumbiji baada ya mafuriko

Ndege ya Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR yenye msaada kwa watu walioathiriwa na kimbunga cha Idai imewasili Maputo, Msumbuji.

Hii ni shehena ya kwanza kati ya tatu kutolewa na UNHCR kwa ajili ya watu waliokumbwa na kimbunga hicho katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema, msaada huo ambao ni pamoja na mahema, mablanketi, vyandarua, na taa za kutumia nishati ya jua utafikishwa kwa watu elfu 30 nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, huku timu za dharura za UNHCR zikitumwa katika nchi hizo tatu.

Mkurugenzi wa UNCHR Kusini mwa Afrika Valentin Tapsoba amesema manusura wa maafa ya kimaumbile katika eneo hilo wanahitaji misaada ya kimataifa. Nchini Msumbiji, misaada hiyo awali kabisa itafikishwa katika eneo la Beira ambalo liliathirika vibaya zaidi kutokana na kimbunga hicho. Maelfu ya watu katika eneo hilo ima wamepoteza maisha au mitaji yao ya kimaisha.

Mafuriko nchini Msumbiji

Zaidi ya watu 700 wamethibitishwa kupoteza maisha hadi hivi sasa kutokana na kimbunga kikali cha Idai kilichopiga eneo la kusini mwa Afrika huku taarifa zikisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka idadi hiyo kutokana na watu wengi kutojulikana waliko.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, uharibifu wa janga hilo la kimaumbile ni mkubwa sana kiasi kwamba, umefika umbali wa kilomita 300 kutoka eneo kilipopiga kimbunga cha Idai.