Wanawake waandamana Comoro kupinga ushindi wa Rais Azali
Makumi ya wanawake katika visiwa vya Comoro wamefanya maandamano hii leo kupinga ushindi wa Rais Azali Assoumani katika uchaguzi wa rais wa hivi karibuni.
Duru za habari zinaarifu kuwa, wanawake 12 waliokuwa katika maandamano hayo wamekamatwa na maafisa wa polisi. Maafisa hao wa polisi wameutawanya mkusanyiko wa wanawake hao waliokuwa wakiandamana kuelekea katika Mahakama ya Juu ya nchi hiyo, kupinga ushindi huo wa Rais Assoumani katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita.
Mashuhuda wamenukuliwa na shirika la habari la AFP wakisema kuwa, taharuki ingali imetanda nchini humo haswa katika visiwa vya Anjouan na Moheli ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na harakati za kutaka kujitenga.
Wapinzani nchini Comoro wanadai kwamba, uchaguzi wa Jumapili iliyopita wa Rais uligubikwa na udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuwazuia waangalizi huru kufuatilia yaliyokuwa yanaendelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura.
Tume ya Uchaguzi ya Comoro CENI ilimtangaza Rais Azali Assoumani kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa Jumapili iliyopita kwa kupata asilimia 60.77 ya kura, matokeo ambayo wapinzani, asasi za kirai na timu za waangalizi zimeyatilia shaka.
Mwezi Julai mwaka jana, Rais Assoumani alishinda kura ya maoni ya kurefusha kipindi cha uongozi wa rais na kukomesha mfumo wa kuongoza kwa zamu baina ya visiwa vitatu vikuu vinavyounda Jamhuri ya watu wa Comoro, hatua ambayo imemfungulia njia ya kusalia madarakani hadi mwaka 2029.