Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Tanzania alionya Bunge
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Tanzania, Profesa Mussa Juma Assad ametahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya hatua ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupasisha azimio la kutofanya kazi naye.
Prof. Assad ametoa indhari hiyo leo Jumatano katika mahojiano na Televisheni ya Taifa (TBC), ambapo ameonya kuwa Bunge linapaswa kuangalia athari ya kile wanachokiamua kwa mapana yake na kwamba, taasisi hiyo ilipaswa kutafuta suluhu ya kile kilichotokea.
Amefafanua kwa kusema, “Mi nafikiri tukae chini tutazame, halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka matatizo ambayo tunaweza kuyasababisha .Wasiwasi wangu ni kuwa, huenda likaja kuwa tatizo kubwa zaidi badala ya kupata suluhisho.“
CAG ameiomba Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kuweka wazi hansadi ya maswali na majibu kuhusu mahojiano yake, yaliyotokana na kosa lililokuwa linamkabili la kulidhalilisha Bunge, ili Watanzania waweza kupima kama uamuzi wa Bunge wa kumtenga ni sahihi au la.
Mapema jana Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka, Emmanuel Mwakasaka aliwasilisha na kusoma bungeni taarifa ya kamati hiyo iliyomuhoji Profesa Mussa Assad, kumtia hatiani, kwa kile ilichokisema kuwa imebaini kauli aliyoitoa kwamba bunge ni dhaifu, alilidhalilisha Bunge la nchi hiyo.
Miongoni mwa wabunge walioupinga vikali uamuzi huo ni mbunge wa Hai, Freeman Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti taifa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.
Tuhuma dhidi ya CAG ziliibuliwa na Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka jana ambapo alisema kwamba, Prof. Assad alilidhalilisha Bunge wakati alipofanya mahojiano na Kituo cha Redio ya Umoja wa Mataifa.