CAG wa Tanzania: Tutaendelea kutumia neno 'Dhaifu' katika ripoti zetu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52759-cag_wa_tanzania_tutaendelea_kutumia_neno_'dhaifu'_katika_ripoti_zetu
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanania, Profesa Mussa Assad amesema kuwa, wataendelea kutumia neno 'dhaifu' katika maeneo tofauti ya ukaguzi wao kulingana na taratibu za kazi hiyo zilivyo na kwamba hata ripoti aliyoiwasilisha leo pia ina neno dhaifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 10, 2019 12:05 UTC
  • CAG wa Tanzania: Tutaendelea kutumia neno 'Dhaifu' katika ripoti zetu

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanania, Profesa Mussa Assad amesema kuwa, wataendelea kutumia neno 'dhaifu' katika maeneo tofauti ya ukaguzi wao kulingana na taratibu za kazi hiyo zilivyo na kwamba hata ripoti aliyoiwasilisha leo pia ina neno dhaifu.

Profesa Mussa Assad ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma ambapo amefafanua masuala mbalimbali yanayohusiana na mahesabu ya serikali ya nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa hatua ya mdhibiti huyo wa hesabu za serikali kulitaja bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani kuwa ni dhaifu kutokana na kushindwa kwake kuchukua maamuzi stahili kwa ripoti zinazowasilishwa na ofisi yake, ilipelekea mvutano mkubwa kati yake na muhimili huo unaohusika na kutunga sheria nchini humo. Kauli hiyo ilikosolewa vikali na Job Ndugai, Spika wa Bunge ambaye alimtaka Profesa Assad kujisalimisha mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka na kwamba kinyume na hivyo angefikishwa kwenye kamati hiyo akiwa amefungwa pingu.

Mgogoro ambao umekuwepo kati ya bunge na CAG

Hata hivyo licha ya CAG kuhojiwa hatimaye tarehe pili ya mwezi huu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad suala ambalo lilikosolewa vikali nchini humo. Akizungumzia baadhi ya kasoro za matumizi mabaya ya fedha CAG hii leo amesema kuwa,  ukaguzi uliofanywa na ofisi yake umebaini kwamba serikali ya Dar es Salam imeshindwa kuchangia Shilingi bilioni 111 katika miradi 10 ya maendeleo kinyume na makubaliano ya wadau wa maendeleo. Aidha Assad amesema kuwa mashirika 14 ya umma nchini Tanzania likiwemo Shirika la Ndege (ATCL) yana matatizo makubwa ya kifedha na kupata hasara kiasi cha kusababisha madeni zaidi ya mitaji kwa zaidi ya asilimia 100. Aidha mashirika mengine ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Lindi), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Bodi ya Utalii Tanzania, Shirika la Dawasco, Kampuni ya Maendeleo ya Nishati ya Joto Tanzania (TGDC) na kadhalika.