Baraza la Usalama la UN lataka kusitishwa mapigano Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kusitishwa mapigano nchini Libya, huku likiziasa pande husika kurejea katika meza ya mazungumzo.
Baraza hilo lilitoa mwito huo jana Ijumaa, ambapo limevitaka vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa kundi linalojiiita Jeshi la Kitaifa la Libya na vile vya Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya visitishe mapigano hayo yanayoendelea kushuhudiwa katika mji mkuu Tripoli.
Dian Triansyah Djani, Rais wa kiduru wa Baraza la Usalama la UN ambaye pia ni Balozi wa Kudumu wa Indonesia katika umoja huo amesema, "Pande husika katika mgogoro wa Libya zinapaswa kusitisha mapigano mara moja, sambamba na kurejea katika mazungumzo ya amani yanayoongozwa na UN."
Wiki iliyopita, Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL kilivitaka pia vikosi vya pande hasimu visitishe kwa muda wa wiki moja mapigano hayo yanayoendelea kushuhudiwa katika mji mkuu Tripoli, wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Aidha kilivitaka viruhusu ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu kwa wale wanaoihitaji, na kuhakikisha kuwa raia wa mji mkuu huo wanaruhusiwa kutembea kwa uhuru katika kipindi hicho cha usitishaji vita.
Tarehe 4 Aprili mwaka huu, Jenerali Haftar alitoa amri kwa wapiganaji wake kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 440 wameshauawa na zaidi ya 2000 wengine wamejeruhiwa tangu yalipoanza mashambulizi hayo, mbali na watu 55 elfu wengine kukimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.