Serikali ya Tanzania: Maduka ya kubadilisha fedha yataanza shughuli zake hivi karibuni
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini humo yataanza shughuli zake hivi karibuni.
Hatua hiyo imekuja baada ya maduka hayo kufungiwa na serikali kwa muda sasa kufuatia operesheni maalumu iliyofanywa na askari wa serikali waliokuwa wakiwasaka wamiliki wa maduka hayo ambao hawajatimiza masharti ya kazi hiyo.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliwatoa khofu wamiliki wa maduka hayo na kuongeza kwamba shughuli hizo zitaanza hivi karibuni. Aidha Majaliwa ameongeza kuwa kile kinachofanywa ni juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya utendajikazi wa taasisi za fedha ambao ni muhimu kufanikisha malengo ya kiuchumi.
“Wamiliki wa maduka ya kubadili fedha yaliyofungwa wawe watulivu. Benki Kuu inakamilisha utaratibu kabla ya kuwaruhusu waendelee na biashara na kuwahudumia wateja wao,” Amesema Majaliwa. Itakumbukwa kuwa, serikali ilifanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka kadhaa ya mkoani Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam na kupeleka akthari ya maduka hayo kupigwa kufuli kwa maelezo kuwa yalikuwa yakifanya kazi kinyume cha sheria. Katika operesheni hizo, maafisa wa serikali walitajwa kuchukua fedha na simu za wamiliki kwa maelezo kuwa watapewa taarifa hapo baadaye. Aidha baada ya maduka hayo kupigwa kufuli, Benki Kuu ya nchi hiyo (BoT) iliwataka wananchi kubadilisha fedha zao kwenye benki za biashara na taasisi za fedha pamoja na maduka ya Shirika la Posta Tanzania.