Serikali ya Libya kuanzisha operesheni mpya kwa kutumia silaha za Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53595-serikali_ya_libya_kuanzisha_operesheni_mpya_kwa_kutumia_silaha_za_uturuki
Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj imetangaza habari ya kupokea zana mpya za kivita, vifaru na magari ya deraya kwa ajili ya kuyatumia katika operesheni zake dhidi ya wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2019 20:51 UTC
  • Serikali ya Libya kuanzisha operesheni mpya kwa kutumia silaha za Uturuki

Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj imetangaza habari ya kupokea zana mpya za kivita, vifaru na magari ya deraya kwa ajili ya kuyatumia katika operesheni zake dhidi ya wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar.

Vikosi vitiifu kwa serikali hiyo inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa vimechapicha picha za silaha hizo mpya za kijeshi katika kurasa zao za mtandao wa kijamii wa Facebook, na baadhi ya silaha hizo zina nembo ya kampuni ya silaha ya Uturuki ya Kirpi.

Msemaji wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya mapema mwezi huu alifichua kuwa, vikosi vyao karibuni vitaanza kupokea zana za kijeshi na misaada ya kibinadamu kutoka Uturuki na nchi nyingine rafiki. 

Haftar ambaye anapata uungaji mkono wa moja kwa moja wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia na Misri, anatumia wapiganaji wake wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya katika kuuhujumu mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kuuteka.

Magari ya kijeshi kutoka Uturuki

Aidha baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa na Italia zimetangaza wazi wazi kuviunga mkono vikosi vya Haftar.

Zaidi ya watu 454 wameuawa na wengine 2154 kujeruhiwa, tokea Aprili 4 wakati wapiganaji wa Haftar walipoanza kuuhujumu mji wa Tripoli.