Freeman Mbowe: Katika matatizo ndani ya chama Lowassa alilegea kuliko mlenda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53602-freeman_mbowe_katika_matatizo_ndani_ya_chama_lowassa_alilegea_kuliko_mlenda
Kiongozi wa chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe amesema kuwa, katika dhoruba za miaka mwili ambazo alizishuhudia wakati akiwa ndani ya chama hicho Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, alilegea kuliko mlenda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2019 03:18 UTC
  • Freeman Mbowe: Katika matatizo ndani ya chama Lowassa alilegea kuliko mlenda

Kiongozi wa chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe amesema kuwa, katika dhoruba za miaka mwili ambazo alizishuhudia wakati akiwa ndani ya chama hicho Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, alilegea kuliko mlenda.

Mbowe amebainisha kwamba, Mzee Lowassa aliyejiunga ndani ya Chadema tarehe 28 Julai 2015 na kupitishwa kuwa mgombea urais wa chama hicho akiungwa mkono na vyama rafiki vya Ukawa, alishindwa kuhimili mikikimikiki za upinzani na kuamua kurejea ndani ya chama tawala CCM tarehe mosi Machi mwaka huu. Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kikao cha ndani cha wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo la Singida Kaskazini. Ameongeza kwa kusema “Tulimwambia mzee wewe kama mgombea wa urais toa kauli, watu wanapigwa risasi, simama kama kiongozi laani. Lowassa wewe ni mgombea urais, watu wamekuunga mkono nchi nzima, umezuiwa kwenda kuwashukuru watu milioni sita, simama kulalamika.” Amesema.

Baada ya Lowassa kurejea chama tawala

Kwa mujibu wa Mbowe, licha ya Lowassa kutakiwa afanye hivyo, alishindwa na badala yake akakaa kimya kwa kuona kuwa ndani ya upinzani kuna misukosuko mingi sambamba na kukhofia kupoteza mali zake. Kiongozi wa chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania ameongeza kuwa, kuna siku Lowassa  alikwenda katika futari mwezi Juni 2017 akatoa kauli kuhusu masheikh waliowekwa kizuizini kwa muda mrefu, “Katika ile futari akatoa neno kuwa serikali ifike mahali iwaachie hawa masheikh na kama wana makosa washtakiwe.” Amesema kuwa, kauli hiyo ilimfanya kuitwa Polisi na kuitikia mwito huo Juni 27 mwaka huo. Mbowe amesema kuwa baada ya kutoa kauli ile kuhusu masheikh na kuitwa na jeshi la polisi "Majira ya saa 11 alinipigia simu, nikwamwambia sisi mbona tunaitwa sana polisi? na tangu siku hiyo mzee hakuongea tena na ikafika wakati akaondoka.” Amesema Freeman Mbowe. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani Tanzania "Chadema sio chama cha mtu, hiki ni chama taasisi, yoyote anaweza kuondoka ndani ya Chadema, ataondoka peke yake akiweza sana ataondoka na mke wake.” Ameongeza.