Khalifa Haftar atishia kuziangamiza meli za Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53630-khalifa_haftar_atishia_kuziangamiza_meli_za_uturuki
Kamanda wa vikosi vinavyojiiita Jeshi la Kitaifa la Libya amewaamuru wapiganaji wake kuishambulia meli yoyote ya Uturuki ambayo itakaribia katika eneo la pwani ya Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 22, 2019 03:21 UTC
  • Khalifa Haftar atishia kuziangamiza meli za Uturuki

Kamanda wa vikosi vinavyojiiita Jeshi la Kitaifa la Libya amewaamuru wapiganaji wake kuishambulia meli yoyote ya Uturuki ambayo itakaribia katika eneo la pwani ya Libya.

Gazeti la al Sharqul Ausat limeripoti kuwa Jenerali Khalifa Haftar ameviamuru vikosi vyake vya baharini kuyalinda maji ya eneo la kandokando ya bandari katika pwani ya Libya lengo likiwa ni kuvizuia vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa vilivyoko Tripoli kupata silaha. Jenerali Khaftar ametoa vitisho hivyo katika hali ambayo Uturuki Jumamosi iliyopita ilishusha melini shehena ya silaha katika pwani ya Tripoli. Msemaji wa serikali ya Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya Fayez al Siraj pia amethibitisha kuwasili silaha hizo. 

Wakati huo huo bunge lenye makao yake katika mji wa Tobruk ambalo linamuunga mkono Khalifa Haftar Jumapili wiki hii lilitoa taarifa na kuzituhumu Uturuki na Qatar kuwa zinawaunga mkono wanamgambo wa al Qaida na Daesh huko Tripoli; na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiadhibu Uturuki kwa kupuuza vikwazo vya silaha ilivyowekewa Libya. 

Wanamgambo wa Daesh nchini Libya

 

Katika upande mwingine, maeneo ya kusini mwa mji mkuu Tripoli yamekuwa na usalama wa kulegalega tangu Jumatatu wiki hii na katika baadhi ya maeneo ya kusini mashariki mwa mji mkuu huo likiwemo eneo la Wadi al Rabi kumeshuhudiwa mapigano ya hapa na pale.