May 22, 2019 03:34 UTC
  • Watu 22 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Chad

Watu wasiopungua 22 wameuawa na wengine 28 kujeruhiwa katika mapigano mapya ya kikabila mashariki mwa Chad.

Taarifa zinasema mapigano hayo yalianza Jumapili  katika maeneo ya  Amkaroka, Amsabarna, and Amsiriye baina ya wakulima wa jamii ya Ouaddai na wafugaji wa jamii ya Kiarabu katika jimbo la Sila mashariki mwa Chad.

Serikali ya Chad imeanzisha kampeni ya kukabiliana na uhasama wa kikabila kwa kuwahimiza wananchi wa jamii zote kuishi pamoja kwa amani.

Mapigano ya kikabila ni jambo la kawaida nchini Chad. Mbali na mapigano ya kikabila, nchi hiyo inasumbuliwa pia na mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram masuala ambayo ni changamoto kubwa kwa serikali ya Chad.

Eneo la Ziwa Chad linapakana na nchi nne za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon. Katika miaka ya hivi karibuni mapigano na vitendo vya uhalifu wa magenge yenye silaha na yenye misimamo mikali kama vile Boko Haram vimeongezeka sana kwenye eneo hilo.

Ingawa jimbo la Borno la nchini Nigeria ndicho kitovu cha vitendo vya kigaidi vya Boko Haram, lakini kuanzia mwaka 2015 genge hilo lilipanua wigo wa mashambulizi yake hadi katika nchi za Niger, Chad na Cameroon.

Tags