Mar 10, 2023 07:16 UTC
  • Boko Haram yafanya mashambulizi ya kushtukiza na kuua 26 Borno, Nigeria

Kwa akali watu 26 wameuawa katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia mashambulio ya kushtukiza yaliyofanywa na magaidi wa kundi la Boko Haram.

Kamishna wa Polisi katika jimbo la Borno, Abdu Umar amesema wanachama wa kundi hilo la wanamgambo jana Alkhamisi walifanya mashambulizi mawili tofauti, ambapo katika hujuma ya kwanza mjini Dikwa waliua wavuvi 25 na kujeruhi mmoja.

Umar ameongeza kuwa, askari polisi mmoja ameuawa katika shambulio la pili la magaidi wa Boko Haram dhidi ya kituo cha polisi katika mji wa Magumeri, umbali wa kilomita 20 kutoka eneo la tukio la kwanza.

Kamishna wa Polisi katika jimbo la Borno amefafanua zaidi kwa kusema, "Boko Haram walishambulia kambi yetu. Walikuwa wengi mno. Tulikabiliana kwa risasi na tukawashinda, ingawaje tumempoteza mmoja wetu."

Wanachama wa Boko Haram

Haya yanajiri siku chache baada ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya uchaguzi wa rais. Kama mtangulizi wake Muhammadu Buhari, Bola Ahmed Tinubu aliyetangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Februari 25 anakabiliwa na kibarua kigumu cha kulitokomeza kundi hilo.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu wapatao 36 elfu na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.

Tags