Dec 27, 2022 07:37 UTC
  • Magaidi wa Boko Haram waua raia 17 kaskazini mwa Nigeria

Vyombo vya habari vya Nigeria vimetangaza kuwa, watu 17 wameuawa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia shambulio lililofanywa na magaidi wa kundi la Boko Haram.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi walivamia kijiji cha Airamne katika jimbo la Borno jana jioni na kuwashambulia vibaya wafugaji hao.

Habari zaidi zinasema kuwa, wafugaji 17 wameuawa katika shambulio hilo, wengine kadhaa wamejeruhiwa huku idadi kubwa ya mifugo yao ikiibiwa na magaidi hao wakufurishaji.

Haya yanajiri siku chache baada ya jeshi la anga la Nigeria kutangaza kuwa limeua zaidi ya magaidi 200 wa Boko Haram katika shambulio la anga la ndege ya kivita ya Super Tucano katika Msitu wa Sambisa wa kaskazini mashariki mwa jimbo hilo la Borno.

Wanamgambo wa Boko Haram

Operesheni hiyo ya jeshi la Nigeria ilifanyika wakati magaidi hao walipokuwa kwenye mkutano maalumu ndani ya msitu wa Sambisa, mkutano ambao uliwashirikisha makamanda wakuu wa ISWAP na Boko Haram wakiwemo wale wanaodai kuacha kushiriki katika mashambulio ya magenge hayo ya ukufurishaji. 

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu wapatao 36 elfu na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.

Tags