Tundu Lissu: Nitarejea Tanzania Septemba 7, sawa na tarehe niliyoshambuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53648-tundu_lissu_nitarejea_tanzania_septemba_7_sawa_na_tarehe_niliyoshambuliwa
Mbunge wa Singida Mashariki wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kuwa atarejea nyumbani tarehe 7 Septemba mwaka huu kutokea nchini Ubelgiji alikoenda kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
May 22, 2019 10:05 UTC
  • Tundu Lissu: Nitarejea Tanzania Septemba 7, sawa na tarehe niliyoshambuliwa

Mbunge wa Singida Mashariki wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kuwa atarejea nyumbani tarehe 7 Septemba mwaka huu kutokea nchini Ubelgiji alikoenda kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Akizungumzia suala hilo Lissu amesema: "Narudi nyumbani (Tanzania) Septemba 7 sawa na tarehe ya kushambuliwa kwangu." Amesema. Aidha rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amesema katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka huu atakuwepo nchini Tanzania. Aidha mwishoni mwa wiki iliyopita mbunge huyo wa Singida Mashariki ambaye kwa sasa anatembea kwa msaada wa gongo moja akizungumza na wapiga kura wake kupitia simu ya Mwenyekiti wa Chadema, (Freeman Mbowe) alisisitiza kwamba atarudi nchini Tanzania Septemba 7 mwaka huu.

Tundu Lissu akiwa na Paul Makonda katikati na Freeman Mbowe miaka michache iliyopita

Tundu Lissu amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa eneo la makazi yake Area D, mjini Dodoma. Mara baada ya kushambuliwa, mwanasiasa huyo  alipelekwa hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyo akahamishiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambapo alipatiwa matibabu hadi Januari 6, mwaka jana na kisha kuhamishiwa nchini Ubelgiji hadi leo.