Rais wa Tanzania: Sasa Zimbabwe iondolewe vikwazo kwani uchumi wake umeboreka
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania sambamba na kumpongeza Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, kutokana na hatua madhubuti za kufanya mageuzi ya uchumi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Rais Magufuli imesema kuwa rais huyo wa Tanzania aliyasema hayo katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mnangagwa katika ikulu yake mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, muda mfupi baada ya Mnangagwa kuingia madarakani hali ya uchumi wa Zimbabwe imeanza kuimarika. Aidha ameongeza kwamba, kwa sasa uchumi wa nchi hiyo unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, na mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 huku mwaka unaofuata ikitajwa kuongezeka hadi wastani wa asilimia 4.4. Ni kutokana na hali hiyo ndipo rais huyo wa Tanzania akaitaka jamii ya kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe, na kwamba vikwazo hivyo vinawaumiza wananchi wakiwemo watoto na wanawake.
Katika sehemu nyingine Rais John Pombe Magufuli ametoa mkono wa pole kwa Wazimbabwe kutokana na kupoteza ndugu zao takribani 400 waliofariki dunia katika mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai kilichoikumba nchi hiyo mwezi Machi mwaka huu. Aidha akizungumzia uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Zimbabwe ulioasisiwa na rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere na rais mstaafu wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Rais Magufuli amesema kuwa, serikali ya Dar es Salaam inatambua na inathamini uhusiano huo wa kihistoria. “Rais Mnangagwa ujio wangu hapa Zimbabwe ni kuthibitisha kuwa urafiki wetu bado upo imara na sisi Tanzania tumejipanga kuuimarisha zaidi, tunataka tufanye biashara zaidi na nyinyi ndugu zetu wa Zimbabwe ili tukuze uchumi wa nchi zetu na kuongeza kipato cha wananchi wetu," Amesema Magufuli. Kwa upande wake Rais Emmerson Mnangagwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake, na amemthibitishia kuwa Zimbabwe inatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao wakiongozwa na Nyerere.