Daesh yadai kuhusika na mauaji ya Congo DR
(last modified Wed, 05 Jun 2019 13:37:58 GMT )
Jun 05, 2019 13:37 UTC
  • Daesh yadai kuhusika na mauaji ya Congo DR

Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuwa ndilo lililohusika na shambulizi lililoua watu kadhaa katika mkoa ulioathiriwa na ugonjwa wa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo la kigaidi imedai kuwa, kundi hilo limelenga askari wa serikali katika mji wa Beni na kuua au kujeruhi watu wasiopungua 25.
Hata hivyo Meya wa mji wa Beni, Modeste Bakwanamaha amesema ni watu 13 tu waliouawa katika shambulizi hilo lililofanyika Jumatatu iliyopita. Bakwanamaha ameongeza kuwa waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) linalodhaniwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la Daesh ndio waliohusika na shambulizi hilo. Amesema wahanga waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine kwa silaha baridi.  
Meya wa mji wa Beni amesema kuwa, kuna uwezekano kwamba shambulizi hilo limefanyika kulipiza kisasi cha mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la serikali dhidi ya wapiganaji wa kundi la ADF na kuuwa wanachana 26 wa kundi hilo. Shambulizi hilo lilifanyika baada ya waasi hao kushambulia kituo cha jeshi katika kijiji cha Ngite karibu na mji wa Beni. 
Kundi la Allied Democratic Forces (ADF) halijawahi kudai kwamba lina uhusiano na lile la kigaidi la Daesh, lakini hivi karibuni Daesh ilidai washirika wake katika kanda ya katikati mwa Afrika wameua makumi ya watu.