S/Kusini: Tumemzuia Riek Machar kwa kuwa anataka kuingiza silaha nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5434-s_kusini_tumemzuia_riek_machar_kwa_kuwa_anataka_kuingiza_silaha_nchini
Serikali ya Sudan Kusini imesema imelazimika kuzuia ndege ya Riek Machar, kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo kutua katika uwanja wa ndege wa Juba kutokana na madai kuwa alitaka kungiza silaha nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2016 03:07 UTC
  • S/Kusini: Tumemzuia Riek Machar kwa kuwa anataka kuingiza silaha nchini

Serikali ya Sudan Kusini imesema imelazimika kuzuia ndege ya Riek Machar, kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo kutua katika uwanja wa ndege wa Juba kutokana na madai kuwa alitaka kungiza silaha nchini humo.

Michael Makuei, Waziri wa Habari wa nchi hiyo amesema Machar alitaka kuingiza bunduki na makombora nchini, hatua ambayo inakiuka makubaliano ya amani yaliyofikiwa na pande mbili hizo. Aidha serikali ya Sudan Kusini imemtuhumu Machar kuwa alitaka kuwasili Juba na vikosi vya askari zaidi, jambo ambalo halipo katika fremu ya makubaliano ya amani.

Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema limetiwa wasiwasi mkubwa na kushindwa Riek Machar kwenda Juba kuchukua nafasi yake ya zamani ya Umakamu wa Rais ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya amani ya nchi hiyo.

Riek Machar alitarajiwa kurejea mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba tangu juzi, lakini msemaji wa kundi lake alisema amechelewesha safari yake hiyo kutokana na sababu za kilojistiki. Jumanne iliyopita, Alfred Ladu Gore, makamu kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini aliwasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba pamoja na ujumbe wa watu 60, katika fremu ya makubaliano ya amani. Gore na ujumbe wake waliwasili siku chache tu baada ya askari 1,370 wa waasi kuwasili mjini Juba, hatua iliyotajwa kuwa ni sehemu ya makubaliano ya amani baina ya waasi na serikali ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili katika nchi hiyo yenye watu milioni 11 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano ya zaidi ya miaka miwili yaliyozuka mwishoni mwa mwaka 2013, miaka miwili tu tangu Sudan Kusini kuwa nchi huru. Mapigano hayo yalichochewa na hatua ya Rais Salva Kiir kumfuka kazi makamu wake Riek Machar kwa madai ya kula njama ya kutaka kumpindua.