FAO: Dagaa ni muhimu katika kumaliza njaa Afrika
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, FAO limesema utafiti mpya umebaini umuhimu mkubwa wa samaki wadogo kama vile dagaa katika kumaliza tatizo la njaa na kuinua kipato kwa wakazi wa bara la Afrika.
Utafiti huo uliochapishwa wiki hii unaonesha kuwa dagaa na samaki wengine wadogo wanaovuliwa mtoni na ziwani ni robo tatu ya samaki wote wanaovuliwa kwenye vyanzo hivyo vya maji barani Afrika.
Hata hivyo utafiti huo unasema licha ya umuhimu wake kiafya na kuwa na kiwango cha juu cha lishe bado hawapatiwi kipaumbele kutokana na thamani yake ndogo kiuchumi ingawa uvuvi wake hauhitaji teknolojia ya hali ya juu.
Hata hivyo FAO inasema ili kuhakikisha kuwa dagaa na samaki wengine wa maji baridi wanapatikana kwa kila mtu ni lazima kufanyike mabadiliko ya kimsingi kiuchumi, kijamii na kisiasa kwenye maeneo husika kuanzia masoko, “kwa sababu mara nyingi huonekana kama ni taka, na sheria zinasema kuwavua ni kinyume cha sheria kwa kuwa uwepo wao unaonekana kuwa ni muhimu katika kuwalinda samaki wakubwa.”
FAO inapendekeza juhudi zaidi za kuwa na takwimu sahihi za uvuvi wa samaki hao wadogo, kutambua hasara za kupuuza thamani yao kiuchumi, kijamii na kwenye lishe na kuhamasisha serikali kuweka kanuni ili kuleta mlingano katika uvuvi.