Kuendelea vitendo vya utumiaji mabavu nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55628-kuendelea_vitendo_vya_utumiaji_mabavu_nchini_sudan_kusini
Licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani huko Sudan Kusini, lakini machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vingali vinaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 27, 2019 06:46 UTC
  • Kuendelea vitendo vya utumiaji mabavu nchini Sudan Kusini

Licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani huko Sudan Kusini, lakini machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vingali vinaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo.

Yasmin Sooka, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ameonyesha wasiwasi mkubwa alionao kuhusiana na vitendo vya utumiaji mabavu sambamba na pande hasimu nchini humo kupuuza makubaliano ya amani ya Septemba 2018.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema wazi kuwa, kutochukuliwa hatua watu wanaohusika na vitendo vya utumiaji mabavu na ubakaji nchini Sudan Kusini ni jambo ambalo limekuwa la kawaida sana na kutia wasiwasi mno, hasa kwa kuzingatia kwamba, wahanga wa ubakaji na utumiaji mabavu hawana mamlaka na nguvu kubwa ya kudai haki zao kupitia vyombo vya mahakama.

Licha ya kuwa Sudan Kusini ina utajiri wa mafuta na madini, lakini inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, kijamii na vilevile mapigano ya ndani.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake Riek Machar

Kujitenga Sudani Kusini na Sudan mwaka 2011 na kuanza vita vya ndani mwaka 2013 nchini humo kumeifanya nchi hiyo igeuke na kuwa moja ya nchi masikini zaidi na yenye kukabiliwa na machafuko zaidi barani Afrika.

Pamoja na kuwa wengi walikuwa na matumaini kwamba, kutiwa saini hati ya makubaliano ya amani Septemba mwaka jana baina ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na kiongozi wa waasi Riek Machar kungepelekea kupungua machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu katika nchi hiyo, lakini hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani vingali vinashuhudiwa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, raia huko Sudan Kusini wamekuwa wakiandamwa na vitendo vya utumiaji mabavu tangu kutiwa saini makubaliano ya amani ya Septemba 2018, kiasi kwamba, machafuko yamewafanya watu 56,000 kuyaacha makazi yao na kukimbilia katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, huku wengine 20,000 wakikimbilia katika nchi nyingine kama Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mapigano Sudan Kusini

Hali hiyo imeufanya mustakabali wa Sudan Kusini kukabiliwa na giza totoro. Watu wengi wana wasiwasi huu kwamba, kuendelea machafuko Sudan Kusini huenda kukasababisha kuvunjwa makubaliano hayo ya amani, na hivyo kuitumbkiiza tena nchi hiyo katika vita na machafuko.

Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa makubaliano ya amani ya Septemba mwaka jana iliamuliwa kwamba, kwa ucahche serikali ya umoja wa kitaifa iwe imeundwa kufikia tarehe 12 Mei mwaka huu, ingawa sasa muda huo umeongezwa kwa miezi sita mingine.

Licha ya kuwa pande hasimu za kisiasa nchini Sudan Kusini zinasisitiiza juu ya kulindwa makubaliano ya amani na kufanyika juhudi za kuboresha hali ya mambo nchini humo, lakini kutokuweko azma na irada thabiti ya kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo kumelifanya suala la kuundwa serikali ya mpito pamoja na mustakabali wa mchakato wa amani kukabiliwa na hatari.

Aidha kuendelea harakati za makundi yya waasi, kuzidi kushuhudiwa mizozo ya kikabila, matukio ya kisiasa huko Sudan na uingiliaji wa kigeni ni mambo ambayo yamekwamisha utekelezwaji wa makubaliano ya amani Sudan Kusini.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Kwa mujibu wa ripoti ya Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan, raia hususan wanawake na mabinti wamekuwa wakiandamwa na vitendo vya ubakaji vilivyoratibiwa katika jimbo la Central Equatoria kusini mwa Sudan Kusini. Aidha kuna wanawake wengi ambao wametekwa. Kwa upande wa nje, kutokea mabadilikko ya kisiasa huko Sudan ndio daghadagha kubwa ya viongozi wa Sudan Kusini.

Roland Marshall, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hilo kwamba: Wasiwasi mkubwa wa Sudan Kusini ni kuwa, serikali mpya ya Khartoum imefuta makubaliano yote ya ardhi na ya mafuta yaliyofikiwa huko nyuma na kutaka kutazamwa upya mikataba hiyo.

Katika mazingira kama haya, kutokea tena vita nchini Sudan Kusini hasa kwa kuzingatia hali ya kiuchumi, kijamii na kisiasa inayotawala nchini humo, itakuwa ni maafa. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wametoa indhari kuhusiana na hilo, lakini inaonekana kuwa, kusaidia juhudi za kurejesha amani, kudhamini miundomsingi ya kiuchumi, kutumwa misaada ya chakula na dawa, kukomeshwa uingiliaji wa kigeni sambamba na kuimarishwa ushirikiano wa Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar katika fremu ya kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani ni mambo ambayo yataandaa uwanja wa kupatikana amani na utulivu huko Sudan Kusini.