Rais wa Burundi akabiliwa na tuhuma za kukiuka haki za binadamu
Kamati ya Umoja wa Mataifa inayochunguza matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi imetangaza kuwa, Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza amekuwa akihusika katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.
Kamati hiyo imewasilisha ripoti yake katika tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binadamu yenye makao yake jijini Geneva Uswisi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, wanasiasa wa upinzani na watu wengine ambao hawashirikiani na serikali kuelekea Uchaguzi wa mwaka 2020, wameuawa au kutekwa.
Hata hivyo serikali ya Burundi imekanusha ripoti hiyo na kusema kwamba, imechochewa na hisia za kisiasa.
Hivi karibuni Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi ilibaini katika ripoti yake kwamba "hali ya hofu" inatawala katika nchi hiyo, ikiwa imesalia miezi minane kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Ripoti hiyo ya Kamisheni ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi imeeleza kuwa, kuna anga ya woga na ukandamizaji dhidi ya wale ambao hawajaonyesha uungaji mkono wao kwa chama tawala CNDD-FDD. Imeongeza kuwa, polisi, askari usalama na jumuiya ya vijana wa chama tawala kwa jina la "Imbonerakure" wameendelea kukiuka pakubwa haki za binadamu, kufanya mauaji, kupoteza watu, kuwatesa raia na kuwabaka kwa makundi watu wanaodaiwa kumpinga Rais Pierre Nkurunziza.
Burundi inaendelea kukumbwa na mgogoro wa kisiasa tangu Rais Pierre Nkurunziza atangaze nia yake ya kuwania katika uchaguzi wa urais mwezi Aprili 2015 kwa muhula wa tatu. Alichaguliwa tena mnamo mwezi Julai mwaka huo huo.