Watu kadhaa wauawa katika shambulizi la bomu Somalia
(last modified Thu, 19 Sep 2019 13:41:05 GMT )
Sep 19, 2019 13:41 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika shambulizi la bomu Somalia

Watu watatu wamethibitishwa kupoteza maisha katika shambulizi la bomu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Duru za habari zimeripoti kuwa, bomu la kutegwa ardhini liliripuka jana jioni katika barabara yenye shughuli nyingi ya Makkatul Mukarrama, na kuua watu watatu na kujeruhi wengine kadhaa.

Mashuhuda wanasema mbunge wa Bunge la Federali la nchi hiyo kwa jina Abdukadir Arabow ameponea chupuchupu katika shambulizi hilo. Habari zaidi zinasema kuwa, bomu hilo liliripuka karibu na gari la mwanasiasa huyo, ambapo walinzi wake wawili wamepoteza maisha.

Kama ilivyotarajiwa, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya Mogadishu. 

Baadhi ya wanachama wa genge la kigaidi la al-Shabaab

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya genge hilo la ukufurishaji kutekeleza shambulizi jingine la kuvizia dhidi ya msafara wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM), lilioua askari 12 wa Burundi. 

Kundi hilo la wanamgambo lilitangaza kuhusika na shambulio hilo na kueleza kuwa, limefanikiwa kuwaua askari 14 wa Burundi katika shambulio hilo.

Tags