Apr 23, 2016 04:20 UTC
  • Rais Zuma wa Afrika Kusini kuitembelea Iran leo

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini anatazamiwa kuwasili nchini Iran Jumamosi ya leo akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi.

Zuma atalakiwa rasmi na Rais Hassan Rouhani wa Iran siku ya Jumapili na viongozi hao wawili watajadili masuala ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili mbali na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.

Katika safari hiyo ya Zuma, nchi mbili zitatiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi.

Zuma pia anatazamiwa kutembelea mji wa kihistoria wa Isfahan siku ya Jumatatu.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rais wa Afrika Kusini kuitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingawa Hayati shujaa Nelson Mandela alitembelea Iran kabla na baada ya urais wake.

Iran ilikuwa mstari wa mbele kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Afrika Kusini kutoka kwenye minyororo wa utawala wa makaburu wabaguzi wa rangi. Baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, nchi hii ilikata uhusiano na utawala wa makaburu na kujiunga katika safu ya mapambano ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini hadi walipopata ushindi.

Tags