Chama cha Kiislamu chaongoza matokeo ya awali ya uchaguzi wa Bunge Tunisia
Matokeo ya awali na yasiyo rasmi ya uchaguzi wa Bunge la Tunisia yanaonesha kuwa chama cha Kiislamu cha al Nahdha kinachoongozwa na Rached Ghannouchi kinaongoza kwa wingi wa viti ikilinganishwa na vyama vingine.
Duru za habari zimeripoti hayo usiku wa kuamkia leo na kusema kuwa, hadi wakati wa kuripotiwa habari hii, chama cha Kiislamu cha al Nahdha kilikuwa kinaongoza kwa kupata asilimia 17.5 ya viti bungeni kikifuatiwa na kile cha Qalb Tunes cha Nabil Karoui kilichopata asilimia 15.6 ya viti bungeni.
Tume Huru ya Uchaguzi ya Tunisia imesema kuwa, asilimia 41.31 ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki kwenye uchaguzi huo wa jana Jumapili.
Huu ni uchaguzi wa pili wa bunge kufanyika Tunisia tangu ilipopasishwa katiba mpya mwaka 2014 na ni uchaguzi wa tatu wa bunge tangu wananchi walipompindua dikteta wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tunisia, chama kinachofanikiwa kupata viti vingi bungeni ndicho kinachopewa jukumu la kuunda serikali kwa kura na idhini ya bunge katika kipindi kisichozidi miezi miwili.
Kama chama kilichoshinda hakitoweza kuunda serikali katika muda uliopangwa, rais wa Tunisia hutumia haki yake ya kikatiba, kumchagua mtu kushika nafasi ya Waziri Mkuu tab'an waziri mkuu huyo analazimika kupigiwa kura na Bunge.
Tarehe 15 mwezi uliopita wa Septemba pia kulifanyika uchaguzi wa rais nchini Tunisia, na hakuna aliyepata kura za kutosha za kumuwezesha kuongoza nchi. Hivyo wagombea wawili, Kaïs Saïed na Nabil Karoui wameingia katika duru ya pili ya uchaguzi huo iliyopangwa kufanyika tarehe 13 mwezi huu wa Oktoba, 2019.