Al-Shabaab yadai kuua watu 6 katika shambulizi la bomu Mogadishu
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limedai kuwa limeua watu sita katika shambulizi la bomu lililolenga ofisi kuu za Kikosi cha Pamoja cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) zilizoko mjini Mogadishu.
Genge hilo la kigaidi limetangaza kuwa, miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo la jana Jumapili ni raia wawili wa kigeni na kwamba watu wengine watano wamejeruhiwa.
Hata hivyo Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, James Swan sambamba na kulaani shambulizi hilo dhidi ya ofisi za wanadiplomasia anasisitiza kuwa hakuna mtu aliyeuawa katika hujuma hiyo lakini watu kadhaa wamejeruhiwa.
Shambulizi hilo limefanyika katika hali ambayo, leo Jumatatu (Oktoba 14) ni maadhimisho ya miaka miwili tangu kundi hilo la wanamgambo litekeleza moja ya mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani, ambapo mamia ya watu waliuawa.
Katika shambulizi hilo, watu zaidi ya elfu moja waliaga dunia baada ya lori lililokuwa limesheheni mabomu kuripuka katika makutano ya barabara ya K-5, eneo lenye shughuli nyingi katika kitovu cha mji mkuu Mogadishu.