Mali yamtia nguvuni mshukiwa wa mlolongo wa mashambulio ya kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5665-mali_yamtia_nguvuni_mshukiwa_wa_mlolongo_wa_mashambulio_ya_kigaidi
Serikali ya Mali imetangaza kuwa imemtia nguvuni mwanachama wa kundi lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ambalo lilidai kuhusika na mashambulio ya kigaidi yaliyoua makumi ya watu nchini humo na katika nchi jirani za Burkina Faso na Ivory Coast.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 23, 2016 16:11 UTC
  • Mali yamtia nguvuni mshukiwa wa mlolongo wa mashambulio ya kigaidi

Serikali ya Mali imetangaza kuwa imemtia nguvuni mwanachama wa kundi lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ambalo lilidai kuhusika na mashambulio ya kigaidi yaliyoua makumi ya watu nchini humo na katika nchi jirani za Burkina Faso na Ivory Coast.

Msemaji wa Wizara ya Usalama ya Mali Amadou Sangho, amesema Fawaz Ould Ahmed alikamatwa siku ya Alkhamisi na vikosi vya usalama na intelijinsia katika mji mkuu Bamako wakati akijiandaa kufanya shambulio jengine.

"Tulimkuta na maguruneti na sanduku dogo lililokuwa na silaha. Alihusika na mashambulio ya Radisson, Hoteli ya Nord Sud, mkahawa wa La Terrasse na Hoteli ya Byblos", amesema Sangho.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Wizara ya Usalama ya Mali, Ould Ahmed ni mwanachama wa al Murabit'un, kundi la wanamgambo lenye uhusiano na Al -Qaeda ya Kaskazini mwa Afrika (AQIM).

Al Murabit'un na AQIM yalitangaza kuhusika na mashambulio yote hayo lakini Sangho amemhusisha Fawaz Ould Ahmed na mashambulio yaliyofanywa nchini Mali tu.

Kabla ya kutiwa nguvuni Ould Ahmed, maafisa wa Mali walitangaza kuwa mwezi uliopita waliwatia mbaroni makumi ya wanamgambo wanaoshukiwa kuhusika ima katika kupanga au kufanya mashambulio ya kigaidi.../