Kinara wa waasi Sudan Kusini atarejea Juba kwa ajili ya mazungumzo
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar anatarajiwa kurejea Juba kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo na Rais Salva Kiir.
Ofisa habari wa rais wa Sudan Kusini Ateny Wek Ateny amesema, mipango inafanywa kwa Machar ambaye yuko nchini Sudan kwenda Juba kwa ajili ya mazungumzo ya amani sambamba na ziara iliyopangwa na wanadiplomasia kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumapili.
Machar ambaye ni kiongozi wa kundi la SPLM-IO yuko katika nchi jirani ya Sudan, na anatarajiwa kufanya ziara yake ya tatu huko Juba tangu akimbilie nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia mapigano yaliyoibuka tena mwezi wa Julai mwaka 2016.
Rais Kiir na hasimu wake mkubwa, Machar wamehimizwa kuheshimu kikamilifu mapatano ya kugawana madaraka kwa shabaha ya kukomesha vita vya ndani vya umwagaji mkubwa wa damu vilivyodumu kwa miaka mitano sasa.
Mapatano hayo yalitiwa saini Septemba 2018 mjini Khartoum, Sudan, mbele ya mataifa ya Sudan, Kenya, Uganda na Djibouti.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.