Oct 19, 2019 13:20 UTC
  • Polisi Nigeria yatumia risasi na mabomu kuvunja Arubaini ya Imam Hussein AS

Polisi nchini Nigeria imetumia risasi hai na mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuvunja matembezi ya amani ya waumini wa Kiislamu waliokuwa wakishiriki maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) katika mji mkuu Abuja.

Mtu mmoja amejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na kopo la bomu la gesi ya kutoa machozi wakati wa maandamano hayo ya jana Ijumaa. Polisi ya Nigeria imefyatua hewani risasi hai kutawanya matembezi hayo, lakini pia imewavurumishia waandamanaji hao mabomu ya kutoa machozi moja kwa moja.

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu yenye makao yake makuu mjini London, Uingereza imekosoa kitendo hicho cha kushambuliwa waandamanaji hao, wakiwemo wanawake na watoto wadogo.

Waaandamanaji hao wametumia jukwaa hilo pia kushinikiniza kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Waandamanaji wakiwa wamebeba picha za Sheikh Ibrahim Zakzaky

Oktoba mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliushambulia msafara wa Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wakishiriki katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS, viungani mwa mji mkuu wa nchi Abuja, na kuua shahidi kumi miongoni mwa waumini hao.

Wimbi la ukandamizaji wa kuchupa mpaka dhidi ya Waislamu nchini Nigeria lilianza mwezi Disemba mwaka 2015, baada ya jeshi la nchi hiyo kuvamia Husseinia ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna na kuua mamia ya Waislamu, mbali na kumtia mbaroni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria, Shiekh Ibrahim Zakzaky, ambaye yuko kizuizini hadi sasa.

Tags