Wanachama 20 wa kundi la ash-Shabab, wauawa nchini Somalia
Maafisa wa serikali ya Somalia wametangaza habari ya kuuawa wanachama 20 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab katika shambulizi lililolilenga gari yao katikati mwa nchi hiyo.
Mohamed Nur Aga Jof, gavana wa mji wa Jalalaqsi, katikati mwa Somalia aliyasema hayo jana Jumamosi na kubainisha kwamba jeshi la serikali ya nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM, wamelishambulia gari lililokuwa limebeba magaidi 20 wa kundi la ash-Shabab katika mji huo na kuwaangamiza wote. Kwa mujibu wa gavana wa mji huo, operesheni hiyo imetekelezwa kwa ushirikiano wa wakazi wa mji huo na kwamba magaidi hao walikuwa wanakusudia kufunga njia zinazouunganisha mji wa Jalalaqsi kwa lengo la kuuzingira na kisha kutekeleza shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi mjini hapo.
Kwa mujibu wa Muhammad Nur, kulijiri mapigano makali kati ya magaidi hao na askari, ambapo hatimaye magaidi hao 20 wa kundi la ash-Shabab waliuawa. Aidha amesema kuwa, askari wa serikali wamefanikiwa kudhibiti bunduki 18 za magaidi. Operesheni hiyo imejiri ikiwa ni siku nne baada ya jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kuwaua wanachama wengine 11 wa kundi la ash-Shabab katika mkoa wa kusini wa Gedo.