Umoja wa Mataifa: Hali ya usalama nchini Somalia bado ni tete
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5674-umoja_wa_mataifa_hali_ya_usalama_nchini_somalia_bado_ni_tete
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, hali ya usalama nchini Somalia bado ni tete.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 23, 2016 22:18 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Hali ya usalama nchini Somalia bado ni tete

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, hali ya usalama nchini Somalia bado ni tete.

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumamosi walitoa taarifa na kulaani mashambulio ya kundi la wanamgambo wa al-Shabab pamoja na hatua ya wanamgambo hao ya kuwatumia vibaya watoto.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema katika taarifa yake hiyo kwamba, licha ya kuchukuliwa hatua mbalimbali za kuboresha hali ya usalama nchini Somalia lakini hali hiyo bado ni tete.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kuweko uratibu zaidi baina ya vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Afrika AMISOM na wanajeshi wa Somalia.

Aidha sehemu nyingine ya taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesifu hatua zilizochukuliwa na AMISOM.

Kikosi cha AMISOM kimekuweko Somalia tangu mwaka 2007 kikijaribu kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambayo inakabiliwa na ukosefu wa amani.

Kundi la wanamgambo wa al-Shabaab lenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda limekuwa likitekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya maafisa wa serikali ya Somalia na vikosi vya kulinda amani.

Huko nyuma kundi la al Shabab lilikuwa linadhibiti maeneo mengi ya katikati na kusini mwa Somalia lakini mwaka 2015 lilipoteza miji mikubwa liliyokuwa linaidhibiti na kubakiwa na baadhi ya maeneo hasa ya vijijini.