Watu 3 wauawa katika shambulio la mtutu wa bunduki Bujumbura, Burundi
Watu waliojizatiti kwa silaha huku wakiwa wamevalia magwanda ya jeshi na polisi wameshambulia klabu moja ya burudani na kuua watu watatu katika mji mkuu wa zamani wa Burundi, Bujumbura.
Naibu Msemaji wa Polisi ya Burundi, Moïse Nkurunziza amesema shambulio hilo lilifanyika jana Ijumaa katika wilaye yenye ulinzi mkali ya Rohero, viungani mwa Bujumbura na kuongeza kuwa, "Watenda jinai wasiojulikana huku wakiwa wamejizatiti kwa bunduki aina ya AK-47 walishambulia watu waliokuwa wakiburudika, ambapo watatu waliuawa na wengine watatu wamejeruhiwa."
Amesema maafisa usalama wameanzisha msako leo Jumamosi wa kuwatafuta wahusika wa jinai hiyo katika mji wa Bujumbura.
Burundi mwaka jana iliuhamishia mji mkuu wake Gitega, katikati mwa nchi, kutoka Bujumbura, mji wa bandari ulioko katika Ziwa Tanganyika.
Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya Polisi ya Burundi kutangaza kuwa imeua wapiganaji 14 na kuwakamata wengine wengi katika mapigano yaliyotokea wilayani Musigati katika mkoa wa Bubanza Magharibi mwa Burundi, yapata kilomita 15 katika mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kundi la waasi la Red-Tabara lilikiri kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa wapiganaji wake ndio waliokabiliana vikali na vikosi vya usalama na ulinzi vya Burundi katika mapigano hayo ya Oktoba 22 na kwamba wanaendelea kuingia nchini Burundi kwa lengo la eti kurejesha utawala wa sheria.