Apr 24, 2016 07:42 UTC
  • Malema: Tuko tayari kupindua serikali ya Zuma hata kwa silaha

Kinara wa upinzani nchini Afrika Kusini ameonya kuwa, wapinzani wako tayari kuipindua serikali ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo hata kwa mtutu wa bunduki.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, Julius Malema, mkuu wa chama cha Economic Freedom Fighters amesema: "Sisi hatuogopa jeshi wala vita, tutapigana na ikibidi tutabeba silaha ili kuiangusha serikali iliyoko mamlakani."

Malema ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Jacob Zuma ameongeza kuwa: "Hivi karibuni subirA itatuishia na hatutakuwa na budi kuing'oa hii serikali hata kwa mtutu wa bunduki."

Wapinzani nchini Afrika Kusini wanamtuhumu Zuma kuwa ni kiongozi fisadi, haswa baada ya Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kumpata na hatia ya kukiuka katiba na kumuagiza kulipa sehemu ya fedha zilizotumiwa katika ukarabati wa nyumba yake binafsi katika eneo la KwaZulu Natal, mradi ambao uligharimu zaidi ya dola milioni 16 za Marekani.

Hata hivyo Rais Zuma alinusurika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni kufuatia kashfa hiyo.

Tags