Sep 29, 2024 14:15 UTC
  • Pretoria: Tunatiwa wasi wasi na mauaji ya kigaidi ya Israel

Afrika Kusini imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja nchini Lebanon, ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza mashambulio ya anga hivi karibuni, na kuua mamia ya raia huku maelfu ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema katika taarifa kuwa: Pretoria inatiwa wasi wasi na kuongezeka kwa "mauaji ya kiholela," hasa mauaji ya kiongozi wa Hizbullah (Sayyid) Hassan Nasrullah na viongozi wengine nchini Lebanon.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kiwango cha majeraha yaliyosababishwa na mashambulizi ya kiholela ya Israel kinatia wasiwasi sana na kwamba jinai hizo zinapasa kushutumiwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

"Mashambulizi kama hayo dhidi ya raia yanajumuisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu za kimataifa," imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa, "vitendo hivi vinazidisha hali ya wasiwasi katika eneo la Mashariki ya Kati na inaonekana kuwa vinalenga kudhoofisha juhudi za kimataifa za amani katika kanda."

Afrika Kusini imesema inasimama pamoja na serikali ya Lebanon wakati huu wa changamoto, na ipo tayari kutoa msaada unaohitajika kufuatia mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema Pretoria inatoa wito kwa wahusika wa "uhalifu uliopangwa" nchini Lebanon kuwajibishwa kupitia "uchunguzi wa kimataifa wenye uwazi."

Tags