Rais Rouhani ampokea rasmi Rais Zuma wa Afrika Kusini
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amempokea rasmi mwenzake wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ikiwa ni safari ya kwanza kwa rais huyo kuitembelea nchi hii tangu baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na nchi zinazounda kundi 5+1.
Akiongoza ujumbe wa watu 180 wakiwemo maafisa wa serikali na wawekezaji, Rais Zuma aliwasili mjini Tehran jana Jumapili, kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais Rouhani ili kujadili masuala ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti.
Marais hao wawili ambao kwa sasa wanakutana katika Ikulu ya Saadabad, kaskazini mwa mji mkuu wa Tehran, wanatazamiwa kujadili masuala ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili, mbali na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa.
Katika safari hiyo ya Zuma, nchi mbili hizi zitatiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi. Kadhalika Rais Zuma anatazamiwa kutembelea mji wa kihistoria wa Isfahan siku ya Jumatatu.
Rais wa Afrika Kusini aliwasili jana hapa nchini, na kulakiwa na Hussein Amir- Abdullahian, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni, anayeshughulikia masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika.