Balozi wa Umoja wa Ulaya atimuliwa nchini Benin kwa kuwachochea wapinzani
Serikali ya Benin, imemtimua balozi wa Umoja wa Ulaya kwa tuhuma za kuhusika katika machafuko ya hivi karibuni na pia kwa kuwachochea wapinzani wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Benin imemtaka Oliver Nette, balozi wa EU nchini humo awe ameondoka Porto-Novo, mji mkuu wa nchi hiyo kabla ya Jumapili ya kesho, na kwamba sababu ya kutimuliwa kwake ni kuhusika kwake katika vitendo vya uharibifu na kuwaunga mkono wapinzani waliofanya ghasia za hivi karibuni. Nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika imekuwa ulingo wa mgogoro wa kisiasa na kijamii tangu mwanzoni mwa Aprili mwaka huu.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya mahusiano ya Benin na Umoja wa Ulaya kuchukuliwa hatua kama hiyo. Licha ya juhudi za EU za kuzuia kushtadi mizozo ya kidiplomasia kati yake na Porto-Novo na kutaka kuwekwa wazi tuhuma zilizotolewa na nchi hiyo kumlenga balozi wake, lakini hadi sasa bado serikali ya Rais Patrice Talon haijatoa majibu yoyote kuhusiana na suala hilo. Suala la kumtimua Oliver Nette, balozi wa EU nchini humo liliwasilishwa katika vikao vya Kamati ya Kiafrika ya Baraza la Ulaya, ambayo ina wadhifa wa kusimamia siasa za kigeni za EU barani Afrika. Inaelezwa kwamba mwaka jana pia serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilimpa masaa 48 Bart Ouvry, balozi wa Umoja wa Ulaya mjini Kinshasa kuhakikisha awe ameondoka ardhi ya nchi hiyo.