Makumi wauawa katika mapigano mapya Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57728-makumi_wauawa_katika_mapigano_mapya_sudan_kusini
Kwa akali watu 67 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyotokea katika jimbo la Western Lakes nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2019 03:59 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano mapya Sudan Kusini

Kwa akali watu 67 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyotokea katika jimbo la Western Lakes nchini Sudan Kusini.

Hayo yameripotiwa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ICRC ambalo limeongeza kuwa, watu 29 waliojeruhiwa kwa risasi wameokolewa na kuondolewa kwa ndege kutoka kwenye eneo la mapigano, yapata kilomita 100 kaskazini mwa eneo la Rumbek.

Kiongozi wa ujumbe wa ICRC nchini Sudan Kusini, James Reynold amesema, watu waliookolewa watapata matibabu katika mji mkuu wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, Juba.

Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa, Idara ya Usalama wa Taifa ya Sudan Kusini imeunda kikosi kipya chenye wapiganaji 10,000 kinyume na makubaliano ya amani.

Wapiganaji watiifu wa Rais Kiir

Ripoti iliyotolewa na timu ya wataalamu wanaofuatilia masuala ya vikwazo dhidi ya Sudan Kusini ya Umoja wa Mataifa imefichua kuwa, kikosi hicho kipya kinajumuisha hata watoto ambao aghalabu yao wamesajiliwa kwa nguvu, na kwamba wapiganaji hao wanapatikana katika ngome za kisiasa na maeneo ya kikabila ambayo Rais Salva Kiir wa nchi hiyo ana ushawishi mkubwa na kukubalika.

Umoja wa Afrika umewapa mahasimu wa kisiasa wa Sudan Kusini Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani, Riek Machar nafasi ya mwisho ya siku 100 ya kuunda serikali ya pamoja, baada ya kushindwa kufanya hivyo tarehe 12 mwezi Novemba.