Libya na Misri wazidi kuzozana baada ya Cairo "kuidhalilisha" Tripoli
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imekasirishwa mno na matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na imetoa majibu makali dhidi ya Cairo ikisema huo ni udhalilishaji kwa taifa la Libya.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetoa tamko rasmi na kulaani matamshi ya Ahmad Hafidh, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Misri aliyetoa matamshi ya kuidhalilisha Libya. Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali hiyo ya Libya inayotambuliwa kimataifa imesema kwenye taarifa yake hiyo kwamba, matamshi hayo ya wizara ya mambo ya nje ya Misri hayakuchunga misingi ya kidiplomasia na ni ya kichochezi.
Hivi karibuni, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Misri aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, Baraza la Uongozi la Libya ambalo linatoa matamko na taarifa za mara kwa mara, linaundwa na watu tisa ambao hata hawajulikani wako wapi.
Itakumbukwa kuwa baraza hilo liliundwa kwenye maafikiano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na kutiwa saini katika mji wa Skhirat, Morocco, tarehe 17 Disemba 2015. Makubaliano hayo ndiyo yaliyounda serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj.
Hata hivyo baadhi ya nchi hasa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi hadi leo zinaendesha kampeni za kufelisha juhudi za kuleta amani na utulivu huko Libya. Nchi hizo zinamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya ambaye anadhibiti eneo la mashariki mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.