Dec 19, 2019 02:33 UTC
  • Makumi wauawa Sudan Kusini licha ya makubaliano ya amani

Zaidi ya watu 100 wameuawa katika mapigano ya kikabila ndani ya mwezi mmoja uliopita nchini Sudan Kusini, licha ya pande mbili hasimu za kisiasa kukubaliana juu ya kuundwa serikali ya umoja kitaifa.

Mapigano ya kikabila yameshtadi vijijini katika maeneo ya katikati na kaskazini magharibi mwa nchi. Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini kimetuma wanajeshi wake katika eneo la Bahr el Ghazal kudhibiti hali, baada ya watu 79 kuuawa katika mapigano ya kikabila na kugombania maji na ardhi ya kulisha mifugo.

Alan Boswell, mtafiti wa Shirika la Kimataifa la Migogoro lenye makao makuu yake mjini Brussels amesema, "Kushtadi mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini kunaonesha kiwango cha changamoto zinazokabili mchakato wa amani ya kitaifa nchini humo."

Haya yanaarifiwa katika hali ambayo, Jumanne hii Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alisema, yeye na aliyekuwa kiongozi mkuu wa waasi Riek Machar wamefikia makubaliano ya kuunda serikali iliyokuwa ikingojewa kwa muda mrefu ya umoja wa kitaifa.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na aliyekuwa kiongozi mkuu wa waasi Riek Machar (kushoto)

Kiir na Machar, ambaye sasa ni kiongozi wa upinzani, walikutana kwa muda wa siku tatu katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba, kuyatafutia ufumbuzi masuala makuu yanayozozaniwa na pande mbili, ambayo yalikwamisha kuundwa serikali ya mseto katika muhula uliokuwa umewekwa wa tarehe 12 ya mwezi uliopita wa Novemba.

Umoja wa Mataifa umewapa viongozi hao wa Sudan Kusini siku 100 kuanzia Novemba 12 wawe wameunda serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

Tags