Kikosi cha Haftar chateka nyara meli ya Uturuki pwani mwa Libya
Kikosi cha linalojiita jeshi la taifa la Libya chini ya uongozi wa Jenerali Khalifa Haftar kimeteka nyara meli ya Uturuki katika maji ya Bahari ya Mediterania na kuipeleka katika bandari ya Ra's Al Hilal huko mashariki mwa Libya.
Kikosi cha Jenerali Haftar kimetangaza kuwa, meli hiyo ya Uturuki ilikamatwa jana tarehe 21 Disemba ikiwa katika maji ya pwani mwa Libya.
Ripoti zinasema meli hiyo ilikuwa na bendera ya Granada ikiongozwa na raia wa Uturuki. Kikoso cha Jenerali Haftar kimetangaza kuwa meli hiyo imepelekwa katika bandari ya Ra's Al Hilal kwa ajili ya uchunguzi na ukaguzi zaidi kwa mujibu wa sheria za kimataifa za usafirishaji wa baharini.
Awali jeshi la Khalifa Haftar lilikuwa limetahadharisha kuwa, litashambulia na kugharikisha meli yoyote ya Uturuki itakayokaribia pwani mwa Libya.
Tarehe 27 mwezi uliopita wa Novemba Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki na Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya walitia saini hati ya maelewano kuhusu suala la kushirikiana katika nyanja za usalama na kijeshi na kuainisha maeneo nyeti katika Bahari ya Mediterania. Makubaliano hayo yamekabiliwa na upinzani mkali wa nchi za kandokando ya bahari hiyo hususan Misri, Ugiriki na Cyprus.
Spika wa Bunge la Misri Ali Abdel Aal amesema kuwa nchi yake haitaruhusu dola lolote la kigeni kucheza katika mipaka yake na Libya na kwamba Cairo inapinga hati ya maelewano iliyotiwa saini na nchi za Uturuki na Libya kuhusiana na ushirikiano wa baharini.
Vilevile serikali ya Ugiriki imemfukuza balozi wa Libya mjini Athens, kufuatia kutiwa saini hati hiyo ya maelewano. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki Nikos Dendias amesema kuwa, kutiwa saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa baharini kati ya serikali za Ankara na Tripoli ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa na kufuatia hali hiyo serikali ya Athens imempa muda wa saa 72 balozi wa Libya nchini humo awe ameondoka katika ardhi ya Ugiriki.