Jeshi la DRC laikabidhi Rwanda waasi 71 wa Kihutu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58041-jeshi_la_drc_laikabidhi_rwanda_waasi_71_wa_kihutu
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeikabidhi Rwanda mamia ya Wanyarwanda wanaohusishwa na kundi moja la waasi la Rwanda linaloendesha harakati zake mashariki mwa DRC.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 22, 2019 14:07 UTC
  • Jeshi la DRC laikabidhi Rwanda waasi 71 wa Kihutu

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeikabidhi Rwanda mamia ya Wanyarwanda wanaohusishwa na kundi moja la waasi la Rwanda linaloendesha harakati zake mashariki mwa DRC.

Msemaji wa Jeshi la Kongo DR katika mkoa wa Kivu Kusini, Kapteni Dieudonne Kasereka amesema leo Jumapili kuwa, waasi 71 wa genge la waasi wa Rwanda la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) pamoja na watu 1,500 wa familia za waasi hao walikabidhiwa maafisa wa serikali ya Rwanda jana Jumamosi, ikiwa ni wiki moja baada ya kukamatwa.

Kasereka amesema waasi hao wa Rwanda pamoja na watu wa familia zao walikuwa wakizuiliwa katika kambi ya jeshi ya Nyamunyunyi, yapata kilomita 30 kutoka Bukavu, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kusini.

Kundi la FDLR liliundwa na wakimbizi wa Kihutu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watustsi katika nchi jirani ya Rwanda.

Waasi wa FDLR mashariki mwa Kongo DR

Septemba mwaka huu, kamanda wa waasi hao wa Kihutu kutoka Rwanda aliyekuwa akisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita, Sylvestre Mudacumura aliuawa kwa kipigwa risasi na askari wa jeshi la Kongo, katika jimbo la Kivu Kaskazini, umbali wa kilomita 60 kutoka katika mji wa Goma.

Kundi hilo linalaumiwa kwa kufanya ukatili na mauaji ya kutisha dhidi ya raia wa maeneo ya mashariki mwa Kongo DR.