Kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi magharibi mwa Afrika
Makundi ya kigaidi ya Boko Haramu na Daesh yamezidisha harakati zao katika eneo la magharibi mwa Afrika.
Katika hatua ya hivi karibuni kundi la kigaidi la Daesh limerusha hewani mkanda wa video likionesha mauaji ya Wakristo 11 katika siku za sherehe ya Krismasi. Hadi sasa utambulisho wa watu hao waliouawa bado haujatangazwa lakini inasemekena kuwa, walikuwa wanaume waliotekwa nyara na kundi hilo wiki chache zilizopita katika mkoa wa Borno wa kaskazini mashariki mwa Nigeria. Taarifa ya kundi la Daesh imesema mauaji hayo yamefanyika kulipiza kisasi cha mauaji ya kinara wa kundi hilo Abu Bakr al Baghdadi na msemaji wake, Abul Hassan al Muhajir. Wiki iliyopita pia kundi hilo lilishambulia kambi ya jeshi katika mkoa wa Soum huko kaskazini mwa Burkina Faso na kuua kwa umati watu wasiopungua 122.

Magaidi wa Boko Haram wameua watu zaidi ya elfu 20 na kuwafanya wakimbizi wengine zaidi ya milioni mbili huko Nigeria, Cameroon, Niger na Chad tangu mwaka 2009 hadi sasa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa hujuma na vitendo vya utumiaji mabavu vya kundi la Boko Haram vimesababisha moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu na kwamba mamilioni ya raia huko Nigeria wanahitaji misaada ya haraka. Kundi hilo la kigaidi limeshadidisha mashambulizi yake katika nchi mbalimbali za magharibi mwa Afrika kwa kulibai kundi la Daesh.

Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kutangaza kuwa makundi ya kigaidi yamewanyonga raia wengi katika jimbo la Borno na kuwateka nyara wengi. Hii ni katika hali ambayo nchi kubwa za magharibi mwa Afrika zikiwemo Niger, Cameroon na Chad kwa muda mrefu zimekuwa zikifanya juhudi za kuyaangamiza makundi ya kigaidi katika eneo hata hivyo hadi sasa nchi hizo hazijafanikiwa pakubwa katika uwanja huo. Kwa kadiri kwamba kushindwa nchi hizo kuendesha mapambano kikamilifu dhidi ya magaidi wa Boko Haram kumepelekea kuenea mapigano katika eneo na kuongezeka hatari ya kupanuka harakati za kigaidi katika nchi nyingine za Kiafrika.
Kuendelea harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika kunaweza kuchunguzwa katika pande mbili za ndani na nje. Kwa upande wa ndani, hakuna hatua zozote za kivitendo zilizochukuliwa katika uwanja huo licha ya nara zinazotolewa na viongozi wa baadhi ya nchi za magharibi mwa Afrika akiwemo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ambaye alitoa ahadi ya kuliangamiza kundi la Boko Haram wakati wa kampeni za uchaguzi. Uhaba wa bajeti, kutokuwa na askari jeshi wenye uzoefu na wa kutosha, hitilafu za ndani, matatizo ya kiuchumi, umaskini na ukosefu wa ajira yote hayo yamesababisha kuendelea kuwepo kundi la Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria na kupanua pia hujuma na mashambulizi yao katika maeneo mengine.
Antoine Glaser Mchambuzi wa masuala ya Afrika anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Ni dhahir shahir kuwa makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka yamefanikiwa kuwashawishi na kuwavutia vijana wenye uwezo mkubwa. Shule elfu mbili zimefungwa huko Burkina Faso. Akthari ya watoto na vijana hawana ajira; na makundi hayo ya uchupaji mipaka yanaweza kwa urahisi kuwaajiri vijana na watoto hao.
Katika upande wa siasa za nje pia uingiliaji wa nchi ajinabi katika eneo umeshadidisha harakati za makundi ya kigaidi. Juhudi za baadhi ya nchi kama Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kujipenyeza huko magharibi mwa Afrika zimepelekea makundi hayo kumiliki silaha na zana za kijeshi kutoka nchi hizo. Aidha kuendelea siasa na uingiliaji wa nchi kama Ufaransa kumeandaa mazingira ya kupanuka harakati za Boko Haram na Daesh magharibi mwa Afrika.
Gazeti la Vanguard linalochapishwa Nigeria limeandika kuwa wanajeshi wastaafu wa Nigeria wanamtuhumu Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuliuzia silaha kundi la kigaidi la Boko Haram. Wanajeshi hao wameitahadharisha serikali ya Ufaransa kwamba kuliunga mkono kundi hilo la kigaidi si kwa maslahi ya Nigeria wala Afrika.

Pamoja na nara zote hizo; makundi ya kigaidi yamezidisha hujuma na mashambulizi yao katika miezi ya karibuni huko Nigeria, Niger, Burkina Faso na katika baadhi ya nchi za eneo; na hii ni tahadhari muhimu kwa jamii ya kimataifa. Inaonekana kuwa Afrika inaendesha vita dhidi ya ugaidi; vita ambavyo vinaweza kufanikiwa tu kwa kushirikiana wa nchi mbalimbali za eneo, kusitishwa uingiliaji wa nchi ajinabi na kwa usaidizi wa taasisi za kimataifa.