Ndege ya kijeshi yaanguka Darfur, Sudan na kuua watu 18
(last modified Fri, 03 Jan 2020 12:29:00 GMT )
Jan 03, 2020 12:29 UTC
  • Ndege ya kijeshi yaanguka Darfur, Sudan na kuua watu 18

Watu 18 wameaga dunia baada ya ndege ya kijeshi kuanguka katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Sudan imesema, ndege hiyo ya kijeshi aina ya Antonov 12 ilianguka jana Alkhamisi, dakika tano baada ya kupaa angani ikitokea Uwanja wa Ndege wa El-Geneina, mkoani Darfur Magharibi, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Chad.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliouawa katika ajali hiyo ni pamoja na wahuduma saba, majaji watatu na raia wanane wakiwemo watoto wanne.

Habari zaidi zinasema kuwa, timu hiyo ilikuwa imeenda katika mkoa huo kutathmini hali ya usalama, kufuatia kuibuka mapigano mapya ya kikabila yalioua makumi ya watu.

Athari za mapigano ya kikabila ya Jumanne iliyopita eneo la Darfur

Mji wa El-Geneina ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Darfur Magharibi umeshuhudia wimbi jipya la mapigano baina ya Waarabu  na wasiokuwa Waarabu katika siku za hivi karibu ambayo yamesababisha kwa akali watu 40 kuuawa.

Serikali mpya ya Sudan imeahidi kumaliza migogoro nchini humo ukiwemo ule wa Darfur ambao umepelekea watu wasiopungua laki tatu kuuawa na wengine milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi tangu mwaka 2003.